SIMBA jana ilizinduka baada ya kushinda bao
1-0 dhidi ya Mafunzo katika mechi ya
michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Simba kwenye
michuano hiyo ya msimu huu baada ya
kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa
Sugar ambapo ilifungwa bao 1-0.
Simba jana ikiwa chini ya Kocha mpya Mserbia
Goran Kopunovic aliyechukua mikoba ya
Mzambia Patrick Phiri, ilionesha soka yenye
kueleweka kidogo tofauti na mechi iliyopita.
Said Ndemla ndiye aliyeifungia Simba bao hilo
katika dakika ya 55 baada ya kuachia shuti kali
lililomshinda mlinda mlango wa Mafunzo,
Hashim Haroun na mpira kujaa wavuni.
Simba itacheza mechi nyingine kesho usiku
dhidi ya JKU ambayo itakuwa mechi ya
mwisho ya kundi na ni ushindi ndio
utakaoivusha raundi inayofuata.
Awali kabla ya mechi hiyo jana, wababe wa
Simba, Mtibwa Sugar nao walibanwa mbavu na
JKU baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Bao la Mtibwa Sugar lilifungwa na Mussa
Hassan ‘Mgosi’ katika dakika ya 20 huku lile la
kusawazisha la JKU lifungwa na Amour Omar
Janja katika dakika ya 72.
Mtibwa inabidi ijilaumu kwani ilikuwa na uwezo
wa kuibuka na ushindi baada ya kuzawadiwa
mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa JKU,
Khamisi Abdallah kunawa mpira eneo la hatari
katika dakika ya 53, lakini Mgosi aliyepewa
dhamana ya kupiga penalti hiyo, alikosa.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni