NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ amesema mfumo unaotumiwa na
Kocha wao Mkuu Hans van der Pluijm
unapendwa na wachezaji, kiasi cha kujituma
na kufanya vizuri.
Akizungumza kwenye runinga ya Azam juzi,
baada ya mechi ya kuwania Kombe la
Mapinduzi kati ya timu yake na Taifa
Jang’ombe kwenye uwanja wa Amaan
Zanzibar, Haroub alisema mfumo unaotumiwa
na Pluijm ni tofauti na ule wa kocha Marcio
Maximo aliyetimuliwa baada ya kuonekana
kutofanya vizuri.
“Mimi binafsi nimeupenda mfumo huu wa
kocha kwa sababu unatufanya tujitahidi na
kujituma kufanya vizuri, unatuletea matokeo
mazuri,”alisema Cannavaro.
Pluijm wakati anajiunga na Yanga mwishoni
mwa mwaka jana, alisema atakuwa anatumia
mfumo wa mashambulizi na kucheza soka la
mvuto ambalo kama wachezaji watacheza
kwa kujiamini watapata matokeo mazuri.
Haroub alisema ikiwa Pluijm ataendelea kukaa
nao kwa muda mrefu kuna uwezekano
mkubwa Yanga kufanya vizuri wakati ujao.
“Kama tutaendelea kuwa na kocha huyu mimi
naamini kuwa kuna mafanikio makubwa mbele,
jambo la muhimu tuombe Mungu atusaidia
kutimiza kile tulichokikusudia,” alisema.
Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Taifa
Jang’ombe ambao walitoka na ushindi wa
mabao 4-0 alisema amefurahishwa na
matokeo hayo na wataendelea kujituma zaidi
kufanya vizuri katika michezo ijayo.
Mchezaji huyo mkongwe wa Yanga alisema
licha ya kikosi chao kucheza soka la kuvutia,
aliwasifia pia timu hiyo ya Jang’ombe ambayo
ipo Ligi daraja la pili Zanzibar kwamba ilijitahidi
kwa uwezo wake.
Mchezaji huyo aliyejiunga na Yanga tangu
mwaka 2005 aliisaidia timu yake kutwaa mataji
ya Ligi katika misimu mitatu ya mwaka 2007,
2009 na 2012.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni