0

SIMBA na Mtibwa Sugar leo zitacheza mechi
ya fainali ya kuadhimisha miaka 51 ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwenye uwanja wa
Amaan mjini hapa.
Fainali hiyo inatarajiwa kuchezwa kuanzia saa
2:15 usiku na mgeni rasmi atakuwa Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Mchezo huo wa fainali ambao umevuta hisia
za mashabiki wa wadau wengi wa soka
unatarajiwa na upinzani wa hali ya juu
kutokana na timu hizo kutaka kulipizana kisasi
hasa kwa upande wa Simba ambao katika
mechi yake ya makundi ilifungwa bao 1-0.
Timu hizo zimefika hatua hiyo baada ya Simba
kuifunga Polisi Zanzibar bao 1-0 na Mtibwa
kuifunga JKU kwa mikwaju ya penalti 7-6
katika mechi za nusu fainali.
Akizungumzia mechi hiyo Kocha Mkuu wa
Simba, Goran Kopunovic alisema anachotaka
ni kushinda ili atwae ubingwa na kulipa kisasi
kwa Mtibwa Sugar ambayo iliifunga bao 1-0
katika mechi ya makundi ya michuano hiyo.
“Mechi itakuwa ngumu lakini nimeitengeneza
timu yangu kuibuka na ushindi kesho (leo)
nataka kujaribu kukwepa kufungwa mara mbili
na Mtibwa,” alisema.
Kwa upande wa kocha wa Mtibwa, Mecky
Maxime alisema timu yake iko vizuri na ana
imani itaibuka na ushindi, ingawa alikiri kuwa
katika wakati mgumu.
“Mechi itakuwa ngumu sana kwetu, kwa
sababu tutataka kushinda ili tusitibue rekodi
yetu na huku Simba nao wakitaka kushinda
kulipa kisasi, lakini wachezaji wangu wanajua
cha kufanya, nimeshawaelkeza,” alisema
mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa.
Mtibwa ndio timu inayofanya vizuri kwenye
msimamo wa Ligi Bara ambapo inaongoza
ikiwa na pointi 16, katika mechi ya raundi ya
raundi ya kwanza ya ligi timu hizo zilitoka sare
ya bao 1-1 kabla Mtibwa haijashinda mabao
3-0 katika mechi ya kirafiki mwishoni mwa
mwaka jana.
Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi ya
michuano hiyo, bingwa atazawadiwa Sh milioni
10, medali za dhahabu na Kombe na mshindi
wa pili atapata Sh milioni tano na medali za
fedha.
Mbali na Mtibwa na Simba, timu nyingine
zilizoshiriki michuano hiyo ni wenyeji Polisi,
JKU, KMKM, Mtende Rangers, Mafunzo na
Shaba za Zanzibar na kwa Tanzania Bara ni
Yanga, Simba, Mtibwa na Azam na KCCA ya
Uganda.

Chapisha Maoni

 
Top