UONGOZI wa klabu ya Simba leo unatarajia
kumtambulisha rasmi kwa wachezaji kocha
Goran Kopunovic baada ya kumsainisha
mkataba wa miezi sita wakiwa Zanzibar.
Kabla ya zoezi hilo la leo viongozi wa Simba
jana walikuwa na mazungumzo marefu na
kukubaliana kila kitu kuhusu mkataba wa
Mserbia huyo aliyekuja kurithi mikoba ya
Mzambia Patrick Phiri.
Habari za ndani zinasema kocha huyo alikuwa
akitaka kupewa mkataba wa mwaka mmoja
lakini uongozi ulimtaka asaini miezi sita ili
amalize ligi ya msimu huu na baada ya hapo
unaweza kumpa mkataba mrefu kama
utaridhishwa na kazi yake.
“Kweli tumekubaliana asaini mkataba wa miezi
sita kwanza ili tuangalie uwezo wake na baada
ya hapo kama tutaridhishwa naye litakuwa ni
suala la kuangalia namna ya kumuongezea
mkataba mpya,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema baada ya kumalizana na
Kopunovic kwa sasa wanaangalia namna ya
kumpata msaidizi wake ama kubaki na
Selemani Matola aliyekuwa akifanya kazi na
Phiri.
“Kwa sasa tunaangalia kama Kopunovic,
atasaidiana na Matola ama tumtafutie msaidizi
wake mwanzoni tulipanga kumleta Jean Marie
Ntagwabila, iliyewahi kufundisha naye timu ya
Polisi Rwanda ili wasaidiane naye,” kilisema
chanzo hicho.
Kopunovic aliwasili nchini juzi asubuhi akitokea
Hungary alipokuwa akiishi ambapo aliwaambia
waandishi wa habari waliofika kwenye Uwanja
wa Ndege ya Kimataifa wa Julius Nyerere
kwamba anataka kuibadilisha Simba kuwa ya
kimataifa.
Aidha kocha huyo alitangaza vita na wachezaji
wote wavivu na watovu wa nidhamu na
kusema anataka kuwa na kikosi chenye
wachezaji wanaojituma ili kuipa timu hiyo
mafanikio.
Alisema anajua Simba ni timu kubwa Tanzania
na atahakikisha anairudisha kwenye kiwango
chake na kufanya vizuri kama ilivyokuwa
zamani wakati ikishiriki mashindano ya
kimataifa.
Kopunovic anakuwa kocha wa tatu tangu
kuingia kwa uongozi mpya chini ya Rais Evans
Aveva, wa kwanza alikuwa Mcroatia Zdravko
Logarusic baadaye walimtimua na kumleta
Phiri naye ameoneshwa mlango wa kutokea
kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo
tangu alipokabidhiwa.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni