TIMU ya soka ya Kagera Sugar jana ilishindwa
kuendeleza makali yake kwenye Ligi Kuu Bara
baada ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi
ya Ruvu Shooting katika mechi iliyochezwa
uwanja wa Mabatini Mlandizi.
Kagera Sugar imepata sare hiyo ikitoka
kuifunga Simba bao 1-0, na hivyo matarajio
yao ilikuwa ni kuibuka na ushindi katika mechi
ya jana.
Habari kutoka Mlandizi zinasema kuwa Kagera
ilikosa mabao mengi ya wazi ambapo
washambuliaji wake walikuwa ama
wanapaisha mpira au inagonga mwamba.
Kwa matokeo hayo, sasa Kagera imefikisha
pointi nne, sawa na Yanga na Azam zilizo
nafasi ya pili na ya tatu. Mtibwa Sugar ndio
inaongoza msimamo ikiwa na pointi 16.
Kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro
mwandishi wetu John Nditi anaripoti kuwa
Polisi Morogoro ilishindwa kuutumia vema
uwanja wake wa nyumbani baada ya
kulazimishwa sare ya bila kufungana na Stand
United ya Shinyanga.
Katika mechi hiyo, timu zote zilishambuliana
kwa zamu huku wachezaji wa Polisi, Said
Bahanuzi na Nicolaus Kabipe wakikosa mabao
mengi hasa kipindi cha kwanza.
Safu ya ulinzi na kiungo ya Stand United
ilicheza vizuri kipindi hicho cha kwanza lakini
washambuliaji wake Haruna Chanongo na
Salum Kamna walikosa mabao ya wazi kwa
mipira yao ama kugonga mwamba ama
kudakwa na kipa wa Polisi, Mohamed Makaka.
Hata hivyo, United ilimaliza pungufu mechi hiyo
baada ya mwamuzi Mathew Akrama wa
Mwanza kumtoa kwa kadi nyekundu Chanongo
kwa madai ya kumtolea lugha chafu
alipompigia filimbi ya kuashiria alicheza rafu.
Hali ilikuwa mbaya pia kwa Wagosi wa Kaya,
Coastal Union ambao walikubali kipigo cha bao
1-0 kutoka kwa JKT Ruvu nyumbani uwanja
wa Mkwakwani Tanga.
Ruvu ilipata bao lake katika dakika ya 38
likifungwa na Samwel Kamuntu katika mechi
hiyo ambayo Coastal ilionekana kuzidiwa.
Matokeo hayo yanaifanya Ruvu kukwea mpaka
nafasi ya tano kwenye msimamo ikiishusha
Coastal kwa kufikisha pointi 13. Coastal ina
pointi 12.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni