0

WATUMISHI wa umma wa ngazi mbalimbali
waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi
wameombwa kuzisoma na kusikiliza kwa
umakini hotuba mbalimbali za Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili
ziwaweke kwenye msingi wa kuwa na maadili
mema, uadilifu na uwazi.
Changamoto hiyo imetolewa na Askofu
Telesphor Mkude wa Kanisa Katoliki Jimbo la
Morogoro, hivi karibuni wakati akizungumza na
gazeti hili kwenye ofisi ya Kanisa Kuu la
Mtakatifu Patrice, mjini Morogoro.
Akijikita katika suala la maadili ya viongozi wa
umma, Askofu Mkude, alisema suala la
kufuata maadili, kuonesha uadilifu na uwazi
katika uwajibikaji wa kuwatumikia wananchi ni
sifa kuu ya kiongozi yoyote yule.
Askofu Mkude alisema ni muhimu kwa
viongozi wetu wakazirejea hotuba mbalimbali
za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, ambaye
wakati wa utawala sifa kuu ya kiongozi ilikuwa
ni mwonekano wake katika maadili na
uzingatiaji wa miiko ya uongozi.
“Nadhani kuna mahali tumeteleza ...viongozi
wetu wengi hawatendi majukumu yao kwa
kufuata maadili, uadilifu na uwazi na hili ndilo
lililotufikisha hapa tulipo...ni budi tukaangalia
wapi tulikotoka na tunaelekea wapi ili
tujisahihishe,” alisema Askofu Mkude.
Hivyo alisema, Mwalimu Nyerere alilijenga taifa
la watu wenye kuwa na uzalendo wa nchi yao
na viongozi walioteuliwa ama kuajiriwa kuwa
watumishi wa umma walifuata maadili ya
utumishi wao tofauti na iliyo sasa.
“ Mwalimu Nyerere alikuwa mwadilifu katika
matendo yake …hakujilimbikizia mali na hata
watoto wake walikuwa ni sawa na watoto wa
watu wa kawaida...na ndiyo maana alikuwa na
uwezo wa kukemea maovu na wakosaji
wakatii,“ alielezea:
“ ...Mwalimu Nyerere alijenga tabia ya
kufuatilia nyendo za viongozi wake na pale
alipoona ama kubaini kiongozi wake
anakwenda kinyume na utaratibu hakusita
kumuita ofisini na kumkanya sambamba na
kumwongoza njia nzuri, “ alibainisha Askofu
Mkude.
Hivyo alisema, kutokana na misimamo hiyo
iliyotokana na uadilifu wake, hotuba zake
alizokuwa akizitoa miaka mingi ya nyuma
zinaporudiwa kwenye redio ama televisheni,
zimekuwa na mvuto na mafunzo ndani yake
kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa mujibu wa Askofu huyo, hivyo ni vyema
viongozi wa sasa pamoja na kuwa na
majukumu mengine ya kikazi, ni jambo jema
pia wakajikumbusha kwa kuzisikiliza kwa
makini na zinaweza kuwarejesha kwenye
mstari wa kuwa waadilifu, wanaofuata maadili
mema ya utumishi wa umma na kujenga zana
ya uwazi na uwajibikaji katika jamii.

Chapisha Maoni

 
Top