0

TIMU ya soka ya Yanga jana ilipaa kileleni
mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya kuifunga
Coastal Union bao 1-0 katika mechi
iliyochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani,
Tanga.
Yanga ambayo Jumapili iliyopita ililazimishwa
sare ya bila kufungana na Ndanda FC, kwenye
Uwanja wa Taifa Dar es Salaam pamoja na
ushindi huo, ilionyesha kiwango kibovu kwa
kuiga mpira uliokuwa unachezwa na wenyeji
wao Coastal Union.
Bao pekee la Yanga katika mchezo huo
lilifungwa katika kipindi cha kwanza na
nahodha wake Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa
kichwa, akiunganisha mpira uliokuwa
umerushwa na Mbuyu Twite dakika ya 11 ya
mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki
wengi wa Jijini Tanga na mikoa jirani.
Kiungo Abdulhalim Humud wa Coastal Union
alikaribia kuisawazishia timu yake bao dakika
ya 39, baada ya kupiga mpira wa adhabu
ndogo nje ya kisanduku cha penalti, lakini
mpira wake ulipanguliwa na kipa wa Yanga,
Ally Mustapha ‘Barthez’ na kumkuta Ramadhan
Salim aliyeshindwa kuukwamisha wavuni na
kuokolewa na walinzi wa vijana hao wa
Jangwani.
Hadi mwamuzi Athuman Lazi wa Morogoro
anapuliza kipyenga cha mapumziko, Yanga
ilikuwa mbele kwa bao hilo la Cannavaro lakini
ilikuwa imezidiwa na Coastal Union ambao
walifanya mashambulizi mengi zaidi kwenye
lango lao na kupoteza nafasi nyingi kupitia kwa
washambuliaji wake, Salimu na Hussein Sued.
Wenyeji Coastal Union walikianza kipindi cha
pili kwa kasi wakiwa na lengo la kusawazisha
bao hilo na kufanya mashambulizi kwenye
lango la Yanga na katika dakika ya 49 Itubu
Imbemu alikosa bao la wazi baada ya kupiga
shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini
Barthez alilipangua na Rajabu Zahiri kuondosha
mpira huo kwenye hatari.
Coastal Union inayofundishwa na kocha James
Nandwa raia wa Kenya, ilijitahidi kupanga
mashambulizi yake na kulishambulia mfululizo
lango la Yanga, lakini washambuliaji wake
Sued na Mnigeria Imbemu walishindwa
kuzitumia vizuri nafasi za kufunga
walizozipata.
Yanga ambao walionekana kucheza kwa
kujihami zaidi huku wakitumia mipira mirefu
dakika ya 55 nusura ipate bao la pili kupitia
kwa Amisi Tambwe aliyekuwa akijiandaa
kuunganisha pasi ya Kpah Sherman lakini beki
wa Coastal Union, Tumba Sued aliutoa mpira
huo nje na kuwa kona.
Beki wa Coastal Union, Tumba alijikuta
akioneshwa kadi ya njano dakika ya 58 kwa
kumchezea vibaya Sherman wa Yanga na
dakika moja baadaye kocha Nandwa alifanya
mabadiliko kwa kumtoa Imbemu na nafasi
yake kuchukuliwa na Keneth Masumbuko
dakika ya 59.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm naye
alikifanyia mabadiliko kikosi chake kwa
kumtoa kiungo Mbrazili Andrew Coutinho na
Tambwe ambao nafasi zao zilichukuliwa na
Hussein Javu na Danny, lakini mabadiliko hayo
hayakubadili matokeo ya mchezo huo.
Zikiwa zimesalia dakika mchezo huo
kumalizika, Sued wa Coastal Union alikosa bao
la wazi akiwa na kipa Barthez baada ya
kutengenezewa pasi safi na Masumbuko, lakini
shuti alilopiga halikulenga lango.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi
22 na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi
Kuu Tanzania bara baada ya kucheza mechi 12
huku ikiipiku Azam iliyopo nafasi ya pili, ikiwa
na pointi 21 na mchezo mmoja kibindoni.

Chapisha Maoni

 
Top