KLABU ya Yanga imewafungulia mashtaka
waliokuwa wachezaji wake watatu, Emmanuel
Okwi, Juma Kaseja na Genilson Santos ‘Jaja’
kwa makosa ya kukiuka sheria na mikataba
yao walipokuwa wakiitumikia klabu hiyo.
Aidha, imewafungulia kesi ya kudai fidia ya Sh
milioni 100.9 wanachama watatu wa Yanga
waliomshtaki Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf
Manji na klabu wakidai uhalali wa katiba ya
Yanga ya mwaka 2010 na 1968.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Yanga, Frank
Chacha alisema Okwi na Jaja wamefunguliwa
mashtaka kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi
za wachezaji ya Shirikisho la Soka Duniani
(FIFA) na Kaseja amefunguliwa kesi katika
Mahakama ya Kazi.
“Wachezaji wote watatu wamekiuka sheria na
hadhi za wachezaji kwa kuvunja mikataba yao
huku wakijua wazi kwamba ilikuwa ni kipindi
cha kazi ambacho kinalindwa, kwa hiyo
mchakato wa kesi utakuwa umekamilika kwa
kipindi cha miezi mitatu,” alisema.
Okwi alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la
usajili akitokea SC Villa ya Uganda baada ya
kushindwana na Etoile du Sahel aliyojiunga
nayo akitokea Simba, kabla ya kurejea tena
Simba.
Chacha alisema Okwi anatakiwa kuilipa Yanga
fidia ya kuvunja mkataba dola za Marekani
milioni moja, fidia ya mazoezi dola za Marekani
100,000, na klabu yake ya Simba ilipe dola
milioni moja na klabu ya Wadi iliyowahi
kufanya naye mazungumzo akiwa na mkataba
na Yanga itatakiwa ilipe dola za Marekani
milioni moja pia.
Alisema pamoja na kutakiwa kulipa fidia hiyo,
pia atatakiwa afungiwe kucheza soka si chini
ya miaka mitano.
Kuhusu barua ya mwanasheria wa Okwi,
Agaba Muhairwe and Co Advocates, Chacha
alikiri kuipokea Desemba 8, mwaka jana,
ikisema kwamba mteja wake anatakiwa alipwe
na Yanga dola za Marekani 62,000 ambazo ni
mshahara na nusu ya fedha alizosaini wakati
anajiunga na klabu hiyo.
Kwa mujibu wa Chacha, barua hiyo imesema
imetokana na hukumu iliyotolewa na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF). Chacha alihoji Okwi
alipata wapi barua ya hukumu ya TFF wakati
Yanga hawajaipata?
Alisema kuwa Yanga waliomba mara mbili
kupewa hukumu ya kesi yao dhidi ya Okwi,
ambapo Novemba 11, mwaka jana walipeleka
barua TFF, bila kujibiwa na Desemba 24, 2014
waliijibu barua ya mwanasheria wa Okwi.
“Sisi baada ya kupata barua hii tulijiuliza
wametoa wapi madai haya, basi tukamjibu
Mwanasheria wa Okwi kwamba
wanachokitaka hakipo, hatujaipata hiyo
hukumu,”alisema.
Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha
sheria na hadhi za wachezaji na kile cha 13
kilitaka Okwi aheshimu mkataba wake wa kazi
pia kifungu cha 12 kinazuia mchezaji kuvunja
mkataba.
Kesi ya Jaja Mbrazili Jaja alijiunga na Yanga
Julai 12, mwaka jana, kwa mkataba wa miaka
miwili na kuitumikia klabu hiyo msimu huu hadi
mechi ya ligi raundi ya saba, ambapo
alikwenda kwao mapumziko na hakurudi tena
kwa madai alikuwa na matatizo ya kifamilia.
Chacha alisema mchezaji huyo aliondoka bila
sababu za msingi huku akijua wazi kuwa ana
mkataba wa miaka miwili na kuigharimu timu
hiyo kusajili mchezaji mwingine.
Alisema amekiuka sheria ya kimataifa na hadhi
za wachezaji kifungu namba 13 ambacho
kilimtaka kuheshimu mkataba wake, pia,
kifungu cha 22 a na b na kwa mujibu wa
kifungu cha 17 cha hadhi ya wachezaji
watamfungulia kesi Fifa, kumdai fidia ya dola
za Marekani 36,000 ikiwa ni mshahara wa
miezi 12 ya mkataba uliobaki.
Pia, atatakiwa kulipa dola milioni mbili kama
fidia ya mazoezi, dola 20,000 kama ada ya
kusaini mkataba. Kesi ya Kaseja Alijiunga na
Yanga msimu uliopita lakini hakucheza kwa
muda mrefu kutokana na kuwekwa benchi.
Chacha alisema kama ilivyokuwa kwa
wachezaji wengine wenye kesi nao Kaseja
alivunja mkataba bila kutimiza muda wake na
Yanga, huku akidai kuwa halipwi ada ya usajili,
hapewi nafasi ya kucheza na hajakatiwa bima,
wakati yote alitimiziwa.
Alisema kifungu namba 14 cha sheria
kinaeleza kuwa mkataba unaweza kusitishwa
kulingana na matakwa ya mchezaji kama
klabu hiyo ilishindwa kumlipa mshahara wa
miezi mitatu, kukosa huduma za chakula na
malazi, na kama Yanga ilishindwa kulipa ada
ya kusaini mkataba wakati wao walitimiza
vyote.
Alisema kutokana na kukiuka hayo, kanuni ya
68 ya Ligi Kuu kifungu kidogo cha 14 inatoa
mamlaka kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za
wachezaji (TFF) kusikiliza na kusuluhisha kesi
kati ya mchezaji na klabu.
Alisema kwa vile mchezaji huyo amevunja
mkataba hata wakipeleka kesi hiyo TFF ni bure
hivyo, kifungu namba 22 kinaruhusu
kumfungulia kesi mchezaji Mahakama ya Kazi
kudai fidia.
Chacha alisema Kaseja atatakiwa kulipa fidia
ya kuvunja mkataba Sh milioni 300, mshahara
wake ambao alikuwa hajautumikia Sh milioni
26.4.
Katika hatua nyingine, Chacha alisema
wameshinda kesi iliyofunguliwa kwenye
Mahakama ya Hakim Mkazi Kisutu dhidi ya
Mwenyekiti wa Yanga na klabu iliyofunguliwa
na wanachama watatu ambao ni Kingwaba
Kingwaba, Juma Mtibwa na Siwema Chiokota.
Alisema kwa kuwa wameshinda kesi hiyo
kibao kitawageukia wanachama hao ambapo
watatakiwa kulipa fidia ya Sh 100,957,000
kama gharama za kesi hiyo na muda
waliopoteza.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni