0


Zitto: Kashfa nne zinakuja
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Kabwe Zitto amesema baada ya
ADVERTISEMENT
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto
amesema baada ya kukamilisha shughuli ya
ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo
Sh306 bilioni zilichotwa, kamati yake sasa
inaelekeza nguvu katika kashfa nyingine nne.
Zitto alisema kamati yake itatumia mwezi huu
na Januari kupitia ripoti nne ambazo zina
masilahi kwa Taifa, ikiwamo ya utoaji wa vibali
vya kuagiza na kuingiza sukari nchini.
Alisema ufisadi katika utoaji wa vibali hivyo ni
mkubwa kuliko sakata la escrow... “Hili
linagusa moja kwa moja maisha ya wananchi,
wamiliki wa viwanda na uzalishaji. Tayari
tumewaita Bodi ya Sukari tujadiliane kwa kina
kuhusu suala hili,” alisema.
Mbali na suala la sukari, alizitaja ripoti nyingine
kuwa ni ya uchunguzi wa ubinafsishaji wa Benki
ya NBC, ripoti maalumu ya Bandari na mikataba
ya gesi.
“Baada ya kazi ya PAC, tunapumzika, kwani
kama unavyojua kazi ilikuwa ngumu, wiki mbili
nilikuwa silali. Kwa kuwa tuna ratiba ya wiki
mbili. Kwa Desemba na Januari tutaanza
kuzifanyia kazi,” alisema Zitto ambaye pia ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Wiki iliyopita, Bunge lilijadili ripoti ya PAC
kuhusu ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow
na kuhitimishwa kwa kuweka maazimio
manane yakiwamo ya kuitaka Serikali
iwawajibishe baadhi ya mawaziri na watendaji
wengine wakuu huku likitaka pia uchunguzi
uendelee kwa wote waliotuhumiwa kupokea
fedha hizo kwa njia moja au nyingine.
Kauli ya Zitto inakuja wiki moja baada ya
wamiliki wa viwanda vya sukari vya Kagera,
Mtibwa na Kilombero kutishia kuvifunga
kutokana na kuviendesha kwa hasara.
Wamiliki hao walisema watafunga viwanda
hivyo kutokana na Serikali kushindwa kuzuia
uagizwaji wa sukari nchini kinyume cha
taratibu.
Mkurugenzi wa Viwanda vya Kagera na Mtibwa,
Seif Seif alisema uagizaji wa sukari kutoka nje
unafanyika kwa ushirikiano wa
wafanyabiashara wakubwa na vigogo serikalini
kinyume cha makubaliano na hivyo kurudisha
nyuma maendeleo ya viwanda.
“Tulikubaliana kwamba Serikali iwe inaagiza
tani 100,000 kutoka nje lakini sukari
inayoingizwa sokoni ni zaidi ya tani hizo. Sukari
tunayozalisha katika viwanda vyetu ipo na
haina pa kwenda,” alisema Seif na kuongeza:
“Leo ukipita katika maduka utakutana na sukari
ya kila aina, wafanyabiashara wanaoagiza
wanawatumia vigogo serikalini kuingiza sukari
wapendavyo, tena bila kulipa kodi,” alisema
Seif.
Kutokana na hali hiyo, Seif alisema
wamelazimika kupunguza wafanyakazi 2,000 na
kubakiwa na 5,000 katika Kiwanda cha Kagera,
Kilombero imepunguza 3,000 na wamebaki
6,000 huku Mtibwa ikiondoa wafanyakazi 3,000.
“Hali ni mbaya, si kama Watanzania
wanavyofikiri. Tukifunga kabisa Watanzania
wengi watakosa ajira kama ambavyo mnaona
wengine wamekosa, hatuwezi kuendelea
kufanya biashara ya hasara ambayo Serikali
inaihalalisha,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Sukari
Kilombero, Balozi Ami Mpungwe alisema: “Hali
ni mbaya, tunaona kuliko kuendelea na hali hii
ni bora tusimame kuzalisha sukari.
“Serikali kama kweli ina dhamira ya kuvifufua
na kuviendeleza viwanda vyetu vya ndani ni
lazima kuvilinda na kupiga marufuku uagizwaji
holela wa sukari kutoka nje.”

Chapisha Maoni

 
Top